Saturday, May 20, 2017


Sefania 3:17
"Yehova Mungu wako yupo katikati yako. Kama Mwenye nguvu, ataokoa.Atakufurahia kwa shangwe. Atanyamaza katika upendo wake. Atakushangilia kwa vilio vya furaha."

Saturday, May 6, 2017

USILIE

Nisomapo  sehemu ya Injili ya Luka  7:13 - 14, nafarijika sana na maneno ya Yesu, "..mama usilie". Yesu anajua msiba wangu, matanga yangu, na aibu yangu. Ni Yesu pekee anayejua chozi langu, sononeko langu na kukata tamaa kwangu. Wengine wote  wanaonizunguka ni waombolezaji. Yesu anajua nipo ndani ya ndoa yangu kwa miaka kumi, lakini sina hata mtoto wa dawa. Yesu anajua  ujane wangu, uyatima wangu. Yesu anajua nipo kitandani  nagaagaa  kwa maumivu na ugonjwa wa muda mrefu, au ninamuuguza kwa gharama kubwa mwenzangu wa ndoa mgonjwa au mtoto.
Ni Yesu pekee anayejua kazini kwangu kuna majungu na upinzani  mkubwa dhidi yangu. Yesu anajua maumivu makubwa niliyonayo kwa vile mwenzangu wa ndoa au mtoto wangu yupo jela. Yesu anajua shida ya mke au mume wangu tuliyetengana kwa muda na uwezekano wa kurudiana ni mdogo. Sauti ya Yesu inaniambia kwa upole katika sikio langu,  huku akiwa amegusa bega langu "usilie.."
Ninamuamini Yesu kwa vile ni yeye pekee anajua chozi ni nini. Juu ya msalaba alilia - "eloi eloi lama sabakthani..", alimlilia rafiki yake Lazaro aliyekuwa kaburini  kwa siku nne. Na aliulilia mji wa Yerusalemu "Dominus flevit"
Bwana Yesu,  kama ulivyomtuliza mjane  wa Naini na kumfufua mtoto wake,  futa CHOZI langu linalonidondoka asubuhi hii. Futa  aibu  yangu. Nijalie  nisikie tena na tena mwaliko wako, "njoni  kwangu ninyi  msumbukao na kuelemewa na mizigo,  nami  nitawapumzisha.."
Ameeeeen  !

Tuesday, April 25, 2017

NI NANI MSHTAKI WA ADUI YAKO?


Siku ya leo ningeomba tafakati yetu tukiongozwa na kitabu cha Esta wakati wa mfalme Ahausero ambapo Esta alichaguliwa kua malkia. “Mfaime akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamria taji ya kifaime kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti” (Esta 2:17). Katika kipindi hiki cha ufalme ndipo amri ilitoka kwa mkuu wa maakida aitwae Hamani bin Hamedatha kua wayahudi wote kuangamizwa (Esta 3:6) akiwemo Malkia Esta pasipo kujua ni myahudi.
Katika maisha yetu ya kila siku kabla ya kuumbwa kwetu Mwenyezi Mungu alitujua kabla “Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nalikujua, na kabala hujazaliwa , nilikutakasa, na kukuweka uwe nabii wa mataifa” (Yeremia 1:5) Hivyo basi anayajua wazi mambo yanayotunyong’onyesha, anayajua vyema ambayo yanatukatisha tamaa na kutueka mbali na yeye. “Hamani” apa huenda ikawa ni hali ya ndoa yako, huenda ikawa ni hali ya kipato chako cha kazi, au huenda ikawa ni uhusiano wako katika famila yako,rafiki jamaa na majirani, Hamani anaweza akawa ni matokeo yako shuleni au matokeo duni ya mipanago yako ya kimaisha, afya yako. Mambo ambayo yanatufanya tuwe mbali na Mwenyez Mungu kwa kutenda dhambi kupitia hayo, kwa namna ya kutegemea mawazo yetu binafsi na kumsahau yeye muweza wa yote.
Mungu anajua kupanda kwako na kushuka kwako, anaijua ilipo huzuni yako na anajua ilipo furaha yako na ndio maana akatupa zawadi pekee ya pendo lake na kwa hilo ashibisha roho zetu. Ametupatia kibali tangu kuumbwa kwetu kwa sura na mfano wake kisha kutufanya wafalme tutawale viumbe vyote, ndege wa angani, samaki wa baharini na wanyama wa porini (Mwanzo 1:26)
Esta kwa kibali alichopata mbele ya mfalme Ahausero aliweza mshtakia amani juu ya mtesi wake. Alimshtakia Hamani juu ya adhma yake ya kutaka kuwaangamiza wayahudi wote pamoja na yeye. aliweza kwa kuongoza na roho wa Mungu kwa sala na toba zilifanywa na wayahudi wote. (Esta 7:1-6)
Anatulika sote kusemezana nae, huu ni mualiko muhim kwetu hasa kwa njia ya imani thabiti iliojengeka mioyo yenu mwetu kwa njia ya kusikia neon lake. Anatualika tumshtaki ‘Hamani’ wetu ni yapi yanayotuangusha, yapi yanayotukatisha tamaa, yapi yanayotueka mbali na pendo lake, ni yapo yanataka kutuanagamiza hasa katika sala. Katika sala tunaweza kushukuru kwa mema mengi Mwenyez Mungu aliotujalia, pia katika sala tunaweza kumueleza masumbuko yetu.          Tuombe
“Nakushukuru Mungu kwa zawadi ya upendo wako kwengu, na kwa ajili ya mema mengi ulionijalia. Mbele zako naziweka shida/masumbuko yangu …(zitaje) nikiamin kua wewe ni mwanzo na mwisho, muweeza wa yote. Nikiomba nguvu mpya na hekima nizidi kupata neema zako nikitegemea msaada wako nikiyashinda yote kadiri ya mapenzi yako. Nikiomba hayo yote kwa njia ya Kristu bwana wetu……….”Amina

Novath Ngowi

Monday, April 24, 2017

Unafahamika mbinguni kwa jina lako

*MWENYEZI MUNGU ANATUFAHAMU KWA MAJINA SIO KWA DHAMBI TULIZOTENDA.*
Katika jamii tunayoishi leo hii, tunafahamu fika kwamba watu wanafahamika kwa namba zaidi kuliko majina. Kwenye vyuo, wanafunzi wanajulikana kwa namba ya usajili! Ukienda hospitalini, kwenye makazi, mitaa, hali kadhalika, ofisi za bima, matokeo ya mitihani kwenye mashule yetu yanatolewa kwa namba na kwingineko. Ukienda jeshini na taasisi za usalama kama vile polisi na mgambo, wahusika wamepewa namba na kwa namba hizo wanajulikana.
Licha ya kwamba sipingani na taasisi ambazo zinawatambulisha watu wake kwa namba, hata hivyo inafaa kugundua tena kwamba jina la Mtu lina maana sana. Kuna nyakati ambazo tunapenda tujulikane kwa majina yetu na sio kwa namba.
Kwa hakika Kanisani, ndipo mahali sawia ambapo tungependa kujulikana kwa majina yetu ingawa pia kama taasisi nyingine, mara kadhaa tumejulikana kwa namba, au tarehe za kuzaliwa na yanayofanana na hayo. Tungelipenda kufahamu fika kwamba Padre au wahudumu wetu wanatufahamu kwa majina yetu, licha ya ukubwa wa jumuiya yetu. Sio lazima padre au wahudumu wetu wafahamu kila kitu kuhusiana na sisi, lakini walau Jina liwe ni mahali pa kuanzia.
Ndugu wapendwa, inapendeza na kuongeza furaha kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu anatufahamu sisi kwa majina yetu na sio kwa dhambi tulizotenda. Kinyume chake shetani anawafahamu wale walio wake kwa dhambi zao. Mwenyezi Mungu anakufahamu wewe binafsi – kwa Jina lako. Maandiko yanatufundisha ukweli huo. “Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya, mwanaume na mwanamke aliwaumba akawabarikia akwaita JINA lao ADAMU, siku ile alipoumbwa. Admu akaishi miaka 130, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita JINA lake SETHI” (rej. Mwa 5: 1-3)
Huenda mpaka sasa hujasikia Bwana akikuita kwa Jina lako, lakini hata hivyo Mwenyezi Mungu anamfahamu kila mmoja wetu kwa Jina kwa sababu alituumba kwa sura na mfano wake, tena anatupenda upeo. Ikiwa anafahamu kila nyota, Je, mimi na wewe tulioumbwa kwa sura na mfano wake, si bora zaidi! “Huihesabu idadi ya nyota, huzipa zote majina (rej. Zab  147:4) Inueni macho yenu juu, mkaone, ni nani aliyeziumba hizi? Aletaye nje jeshi lao kwa hesabu, aziita zote kwa majina, kwa ukuu na uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake, hapana moja isiyokuwapo mahali pake. (rej Isa 40:26).
Hapa ni baadhi ya aya kutoka kwenye Maandiko Matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu anatufahamu sisi kwa majina yetu na si vinginevyo:
👁Lakini sasa Bwana amekuhuluku, ee Yakobo, Yeye aliyekuumba, ee Israel asema hivi, usiogope maana nimekukomboa, nimekuita kwa Jina lako, wewe u-wangu.” (rej Isa 43:1-28).
✍​​​​​Upitapo katika maji mengi, nitakuwa pamoja nawe, na katika mito, haitakugharikisha, uendapo katika moto, hutateketea, wala mwali wa moto hautakuunguza (rej. Isa 43:2).
✍​​​​​Kila mmoja anayeitwa kwa jina langu, niliyemuumba kwa ajili ya utukufu wangu, mimi nimemuumba, naam, mimi nimemfanya (rej. Isa 43:7).
✍​​​​​Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake, naye huwaita kundoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje (rej. Yn 10:3).
✍​​​​​Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi. Kama vile Baba anijuavyo mimi, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo (rej. Yn 10:14-15).
✍​​​​​Kwa kuwa umekaza kunipenda, nitamwokoa na kumweka palipo juu, kwa kuwa amenijua Jina langu (rej. Zab 91:14).
✍​​​​​Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nalikujua, na kabla hujazaliwa, nilikutakasa, na kukuweka uwe nabii wa mataifa (rej. Yer 1:5).
✍​​​​​Bwana akamwambia Musa, nitalifanya neno hili ulilolinena, kwa maana umepata rehema mbele zangu, nami nakujua Jina lako (rej. Kut 33:17).
✍​​​​​Bwana aonaye sirini atakujazi (rej. Mt 6:4-8).
Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)

Monday, April 10, 2017

Tafakari


2Nyakati20:6
"akasema, Ee BWANA, Mungu wa baba zetu, si wewe uliye mbinguni? tena si wewe utawalaye falme zote za mataifa? na mkononi mwako mna uweza na nguvu, asiweze mtu yeyote kusimama kinyume chako"
Mfalme Yehoshafati alipovamiwa aliwakusanya watu wake,wakafunga na kuomba wakimlilia Mungu na kumkumbusha Mungu juu ya nguvu na uweza wake. Nasi pia chochote kilicho kikwazo mbele yetu,tumkumbushe Mungu kwa kufunga na kuomba.
MKUMBUSHE MUNGU.

Sunday, April 9, 2017

Karibu Blogu ya Tumaini Jipya


Karibu katika ukurasa huu wa blogu uitwao TUMAIN JIPYA. Awali ya yote ningependa kumshukuru mwenyezi  Mungu  kwa wingi wa neema na rehema na kwa zawadi kubwa ya uhai aliotujalia mimi na wewe na watu wake wote kwa ujumla. Katika safari ya maisha hapa duniani alitupatia zawadi hii ya uhai ili tuweze kumjua  yeye , tumpende, tumtumikie yeye tukiwa hapa na siku ya mwisho baada ya yote turudi kwake  (Yn 14:3). Tumepata nafasi kubwa kuwa viumbe wa kipekee, tulioumbwa kwa sura na mfano wa mwenyezi Mungu, kisha akatufanya wafalme wenye kutawala vyote samakiwa baharini, ndege wa angani na wanyama na vyote (Mwanzo 1:26). Kwa namna hiyo tumekabidhiwa wajibu wa kutumikiana sisi kwa sisi, tukikumbushana kazi ya wokovu, kupendana, kushirikishana kwa kutiana moyo katika kila changamoto za kimaisha katika safari yetu ya hapa duniani, tukijua ya kwamba ipo tuzo kwa kupigana vita vilivyo vizuri. (2Timotheo 4:8)
Zipo changamoto nyingi za kimaisha tunazopitia kila siku, kubwa na ndogo, zote hizi zipo kwa namna ya kutujenga kwa akututia nguvu na kutukumbusha kua yupo Baba aliesimama nasi na kupigana kwa ajili yetu sisi tukiwa na jukumu la kuilinda Imani, “Lakin mwenye kuvumilia hata mwisho, ndie atakaeokoka’’ (Mt 24:13)
Ningependa kukwambia kua lipo TUMAINI JIPYA, ipo amani katika familia yako, lipo tumaini katika kazi yako, upo ushindi  katika masomo yako, upo upendo katika ndoa yako, upo ushindi katika ndoto zako. Kama ilivyoandikwa kwenye kitabu cha nabii Isaya 41:10 “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkonowa kuume wa haki yangu”. Tusifadhaike mioyoni mwetu, kwa Yesu Kristu ipo faraja, lipo pumziko na ushindi.
Ningependa kukukaribisha tena, tukishirikishana upendo wa Kristu na kuonja raha ya TUMAINI JIPYA chini ya njia ya msalaba kwa masomo na tafakari za biblia.
  
       Karibu!

Msaada wa Mungu

"Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, 'Usiogope, mimi nitakusaidia"
                                                          Isaya 41:13

Saturday, April 8, 2017


MASOMO YA MISA, APRILI 9, 2017
DOMINIKA YA MATAWI

SOMO 1
Isa. 50:4 – 7

Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

Neno la Bwana… Tumshukuru Mungu.

WIMBO WA KATIKATI
Zab. 22:7 – 8; 16 – 17a; 18 – 19; 22 – 23 (K)22:1

(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

Wote wanionao hunicheka sana
Hinifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
Husema: Umtegemee Bwana; na amponye;
Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. (K)

Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga;
Yamenizua mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. (K)

Wanagawanya nguo zangu,
Na vazi langu wanalipigia kura.
Nawe, Bwana, usiwe mbali,
Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)

Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
Ninyi mnaomcha Bwana msifuni
Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni. (K)

SOMO 2
Flp. 2:6 – 11

Ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

SHANGILIO
Flp. 2:8 – 9

Kristu alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.

INJILI
Mt. 26: 14 – 27: 66
 (Historia ya Mateso ya Bwana)
''Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu''
(Isaya 41:10)

Sefania 3:17 "Yehova Mungu wako yupo katikati yako. Kama Mwenye nguvu, ataokoa.Atakufurahia kwa shangwe. Atanyamaza katika upendo wake...