*MWENYEZI MUNGU ANATUFAHAMU KWA MAJINA SIO KWA DHAMBI TULIZOTENDA.*
Katika jamii tunayoishi leo hii, tunafahamu fika kwamba watu wanafahamika kwa namba zaidi kuliko majina. Kwenye vyuo, wanafunzi wanajulikana kwa namba ya usajili! Ukienda hospitalini, kwenye makazi, mitaa, hali kadhalika, ofisi za bima, matokeo ya mitihani kwenye mashule yetu yanatolewa kwa namba na kwingineko. Ukienda jeshini na taasisi za usalama kama vile polisi na mgambo, wahusika wamepewa namba na kwa namba hizo wanajulikana.
Licha ya kwamba sipingani na taasisi ambazo zinawatambulisha watu wake kwa namba, hata hivyo inafaa kugundua tena kwamba jina la Mtu lina maana sana. Kuna nyakati ambazo tunapenda tujulikane kwa majina yetu na sio kwa namba.
Kwa hakika Kanisani, ndipo mahali sawia ambapo tungependa kujulikana kwa majina yetu ingawa pia kama taasisi nyingine, mara kadhaa tumejulikana kwa namba, au tarehe za kuzaliwa na yanayofanana na hayo. Tungelipenda kufahamu fika kwamba Padre au wahudumu wetu wanatufahamu kwa majina yetu, licha ya ukubwa wa jumuiya yetu. Sio lazima padre au wahudumu wetu wafahamu kila kitu kuhusiana na sisi, lakini walau Jina liwe ni mahali pa kuanzia.
Ndugu wapendwa, inapendeza na kuongeza furaha kufahamu kwamba Mwenyezi Mungu anatufahamu sisi kwa majina yetu na sio kwa dhambi tulizotenda. Kinyume chake shetani anawafahamu wale walio wake kwa dhambi zao. Mwenyezi Mungu anakufahamu wewe binafsi – kwa Jina lako. Maandiko yanatufundisha ukweli huo. “Siku ile Mungu alipoumba mtu, kwa sura ya Mungu alimfanya, mwanaume na mwanamke aliwaumba akawabarikia akwaita JINA lao ADAMU, siku ile alipoumbwa. Admu akaishi miaka 130, akazaa mwana kwa sura yake, kwa mfano wake, akamwita JINA lake SETHI” (rej. Mwa 5: 1-3)
Huenda mpaka sasa hujasikia Bwana akikuita kwa Jina lako, lakini hata hivyo Mwenyezi Mungu anamfahamu kila mmoja wetu kwa Jina kwa sababu alituumba kwa sura na mfano wake, tena anatupenda upeo. Ikiwa anafahamu kila nyota, Je, mimi na wewe tulioumbwa kwa sura na mfano wake, si bora zaidi! “Huihesabu idadi ya nyota, huzipa zote majina (rej. Zab 147:4) Inueni macho yenu juu, mkaone, ni nani aliyeziumba hizi? Aletaye nje jeshi lao kwa hesabu, aziita zote kwa majina, kwa ukuu na uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake, hapana moja isiyokuwapo mahali pake. (rej Isa 40:26).
Hapa ni baadhi ya aya kutoka kwenye Maandiko Matakatifu yanayodhihirisha kwamba Mungu anatufahamu sisi kwa majina yetu na si vinginevyo:
👁Lakini sasa Bwana amekuhuluku, ee Yakobo, Yeye aliyekuumba, ee Israel asema hivi, usiogope maana nimekukomboa, nimekuita kwa Jina lako, wewe u-wangu.” (rej Isa 43:1-28).
✍Upitapo katika maji mengi, nitakuwa pamoja nawe, na katika mito, haitakugharikisha, uendapo katika moto, hutateketea, wala mwali wa moto hautakuunguza (rej. Isa 43:2).
✍Kila mmoja anayeitwa kwa jina langu, niliyemuumba kwa ajili ya utukufu wangu, mimi nimemuumba, naam, mimi nimemfanya (rej. Isa 43:7).
✍Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake, naye huwaita kundoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje (rej. Yn 10:3).
✍Mimi ndimi mchungaji mwema, nao walio wangu nawajua, nao walio wangu wanijua mimi. Kama vile Baba anijuavyo mimi, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo (rej. Yn 10:14-15).
✍Kwa kuwa umekaza kunipenda, nitamwokoa na kumweka palipo juu, kwa kuwa amenijua Jina langu (rej. Zab 91:14).
✍Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako nalikujua, na kabla hujazaliwa, nilikutakasa, na kukuweka uwe nabii wa mataifa (rej. Yer 1:5).
✍Bwana akamwambia Musa, nitalifanya neno hili ulilolinena, kwa maana umepata rehema mbele zangu, nami nakujua Jina lako (rej. Kut 33:17).
✍Bwana aonaye sirini atakujazi (rej. Mt 6:4-8).
Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap,
Mwenge Catholic University (MWECAU-MOSHI)