Saturday, May 20, 2017


Sefania 3:17
"Yehova Mungu wako yupo katikati yako. Kama Mwenye nguvu, ataokoa.Atakufurahia kwa shangwe. Atanyamaza katika upendo wake. Atakushangilia kwa vilio vya furaha."

Saturday, May 6, 2017

USILIE

Nisomapo  sehemu ya Injili ya Luka  7:13 - 14, nafarijika sana na maneno ya Yesu, "..mama usilie". Yesu anajua msiba wangu, matanga yangu, na aibu yangu. Ni Yesu pekee anayejua chozi langu, sononeko langu na kukata tamaa kwangu. Wengine wote  wanaonizunguka ni waombolezaji. Yesu anajua nipo ndani ya ndoa yangu kwa miaka kumi, lakini sina hata mtoto wa dawa. Yesu anajua  ujane wangu, uyatima wangu. Yesu anajua nipo kitandani  nagaagaa  kwa maumivu na ugonjwa wa muda mrefu, au ninamuuguza kwa gharama kubwa mwenzangu wa ndoa mgonjwa au mtoto.
Ni Yesu pekee anayejua kazini kwangu kuna majungu na upinzani  mkubwa dhidi yangu. Yesu anajua maumivu makubwa niliyonayo kwa vile mwenzangu wa ndoa au mtoto wangu yupo jela. Yesu anajua shida ya mke au mume wangu tuliyetengana kwa muda na uwezekano wa kurudiana ni mdogo. Sauti ya Yesu inaniambia kwa upole katika sikio langu,  huku akiwa amegusa bega langu "usilie.."
Ninamuamini Yesu kwa vile ni yeye pekee anajua chozi ni nini. Juu ya msalaba alilia - "eloi eloi lama sabakthani..", alimlilia rafiki yake Lazaro aliyekuwa kaburini  kwa siku nne. Na aliulilia mji wa Yerusalemu "Dominus flevit"
Bwana Yesu,  kama ulivyomtuliza mjane  wa Naini na kumfufua mtoto wake,  futa CHOZI langu linalonidondoka asubuhi hii. Futa  aibu  yangu. Nijalie  nisikie tena na tena mwaliko wako, "njoni  kwangu ninyi  msumbukao na kuelemewa na mizigo,  nami  nitawapumzisha.."
Ameeeeen  !

Sefania 3:17 "Yehova Mungu wako yupo katikati yako. Kama Mwenye nguvu, ataokoa.Atakufurahia kwa shangwe. Atanyamaza katika upendo wake...